Tuesday, December 6, 2011

Maasakofu Wadaiwa Kutumia HIRIZI kuvuta Waumini...!!!

Mchungaji huyo alitoa tuhuma hizo  hivi karibuni alipokuwa akifanya mahojiano maalum na gazeti hili kuhusiana  na tukio la hivi karibu la askofu mmoja wa Kinigeria kukamatwa  na madawa ya kulevya.
Mtikila alishauri kusiwepo na suluhu wala msamaha kwa askofu huyo bali sheria ichukue mkondo wake pale itakapothibitika mahakamani kwamba amefanya uhalifu huo.

Mchungaji Mtikila ambaye pia ni kiongozi wa chama cha siasa cha Democratic Party (DP) alisema kwa sasa viongozi wengi wa dini hawafanyi kazi walizoagizwa na Mungu bali wanayatumia makanisa kama sehemu za biashara na kufanyia mambo machafu.

“Ni kweli hatukatai mtu kuanzisha kanisa lakini basi afanye kazi ya Mungu,  siyo kuchanganya na biashara nyingine, ndiyo maana ninasema kwamba wachungaji  wengine  wanafanya kazi ya  Mungu kwa  miujiza ya hirizi,” alisema mchungaji huyo bila ya kutaja majina ya watumishi wenye tabia hiyo.

Akifafanua zaidi, Mtikila  alisema kama mchungaji huyo wa Kinigeria anahusika na biashara hiyo, ni wazi kwamba alikuwa na  mtandao mrefu na lazima serikali itumie kikosi kazi kudhibiti madawa ya kulevya ili kusafisha hali hiyo.
Kuhusiana na madai ya Wakristo au viongozi wa makanisa ya kiroho kutumia hirizi katika shughuli zao za kidini, gazeti hili liliongea  na baadhi ya viongozi wa makanisa hayo ambao walikuwa na haya ya kusema:

MZEE WA UPAKO
Mchungaji Mkuu wa Kanisa la Maombezi la Kibangu jijini Dar, Anthony Lusekelo, ‘Mzee wa Upako’ alisema: “Mungu alikuwa wazi kuhusu uchawi na uzinzi na akaamuru kwamba mtu anayejishughulisha na mambo hayo apigwe mawe hadi kufa.


“Biblia takatifu inakataza Mkristo kujihusisha na uchawi na inasema wazi kuwa mfuasi wa Kristo asiende kwa wapunga pepo yaani wachawi. Nawashauri watu wasome Kitabu cha Kutoka, watanufaika zaidi kuhusu makatazo hayo ya Mungu juu ya uchawi.”

NABII FLORA
Naye Nabii Flora Peter wa Kanisa la Huduma ya Maombezi la jijini Dar amekanusha kuwepo kwa kitu kama hicho kwa kusema kwamba  mtumishi wa Mungu anayetumia nguvu za giza ‘hirizi’ ana imani ndogo kwani hakuna uchawi unaoshinda nguvu ya Yesu.

ASKOFU KAKOBE
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship la jijini Dar, Zachary Kakobe ambaye sasa anajulikana kama mhubiri wa injili wa kimataifa amesema Mkristo safi kamwe hawezi kutumia hirizi ya aina yoyote.
“Wapo watu wanaotegemea kulindwa na hirizi au mafundo, kwa Kiingereza huitwa ‘charm’. Hii ni kazi ya Shetani na ni chukizo kwa Mungu.

“Wakristo tunalindwa na nguvu ya Mungu kwa njia ya imani,” alisema Askofu Kakobe na kuwaomba watu wasome Kitabu cha Ezekiel 13, mstari wa 18-20 au Kumbukumbu la Torati 18, mstari wa 10-12 ambapo ufafanuzi umetolea kuhusu suala hilo la uchawi.

MCHUNGAJI JOHN SAID
Kwa upande wake, Mchungaji John Said wa Kanisa la Victorious la Mabibo External jijini Dar alisema:
“Hirizi za aina yoyote ni makatazo kwa Mungu, anayesema kuna wachungaji wanatumia hirizi kuvuta watu anakosea sana, kwa sababu anajua kuwa watumishi wa Mungu hawawezi kufanya hivyo,” alisema Mchungaji John.


NABII JOSEPHAT MWINGIRA
Nabii na Mtume Josephat Mwingira wa Kanisa la Efatha la Dar, alipofuatwa kanisani hakupatikana  lakini katika mahubiri yake amekuwa akikemea sana wachawi.

Inadaiwa kuwa wengi walioingia kanisani kwa Mwingira kwa lengo la kumjaribu wamekuwa wakiumbuka, kwani amekuwa akisema wazi kwamba wanashindwa kwa jina la Yesu.

NABII ONESMO NDEGI
Nabii Onesmo Ndegi wa Kanisa la Living Water la jijini Dar hakupatikana, japokuwa naye amekuwa akikemea mara kwa mara imani za kishirikina na kuwaelekeza waumini kumfuata Kristo ili waokolewe.

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Uplink Servers Technology | Bloggerized by Kwetu Bongo Online Magazine