Tuesday, December 6, 2011

Ni kweli soda mbaya kuliko sigara?



Wiki iliyopita tulianza makala haya kwa kuangalia madhara yatokanayo na unywaji wa soda kwa wingi ambapo tuliona kuwa kiwango cha ‘fructose’ kinachowekwa kwenye vinywaji vingi baridi na hasa soda ni kikubwa. Tafiti nyingi zinaonesha kuwa ‘fructose’ nyingi ina madhara mwilini na huwa chanzo cha magonjwa ya moyo, kisukari na ini. Wiki hii tunaendelea na sehemu ya mwisho kwa kuangalia athari nyingine, endelea…

NI KWELI SODA HUSABABISHA VURUGU?
Ni ukweli unaojulikana wazi kuwa lishe duni, hasa ile yenye kiasi kingi cha sukari ina athari kubwa kiakili. Utafiti uliofanywa hivi karibuni na kuchapishwa kwenye Jarida la ‘Psychology Today’ nchini Marekani, umebaini kuwepo kwa uhusiano mkubwa kati ya utumiaji wa sukari na hatari ya mtu kupatwa na mfadhaiko wa kiakili (depression) na ukichaa (schizophrenia).

Mlo wenye kiasi kingi cha sukari na ‘fructose’ kwenye vinywaji kama soda, husababisha uzalishaji mwingi wa ‘insulin’ ambako kunaweza kusababisha kushuka kwa kiasi cha sukari mwilini na kusababisha matatizo mengine yanayoweza kumfanya mtu kuwa na hasira, hamaki na mshituko.

Utafiti mmoja uliofanywa mwaka 1985 na kuchapishwa kwenye Jarida la ‘Abnormal Psychology’ nchini Marekani, ulibaini kuwa upunguzaji wa matumizi ya sukari una manufaa mengi katika hisia za mtu.

Katika utafiti huo, vijana waliokuwa na tabia mbaya na vurugu, walifanyiwa utafiti wa miezi mitatu kwa kupewa milo ya aina mbalimbali isiyokuwa na sukari na ilionekana kuwepo kwa mabadiliko makubwa ya kitabia kwa asilimia 44, ukilinganisha na wale waliokula milo au vinywaji vyenye sukari nyingi.

HIVYO NI KWELI SODA INA ATHARI KWENYE TABIA YA MTOTO?
Ni kweli soda zina athari kwenye tabia ya mtoto. Utafiti uliofanyika una sapoti maelezo haya kwa kubainisha kuwa unywaji wa mara kwa mara wa vinywaji baridi vyenye sukari, umehusishwa na vitendo vya vurugu kwa silimia 9 hadi 15 hata zikitumika jitahada zingine za kudhibiti hali hiyo.

WATAFITI WANAMALIZA KWA KUSEMA:
“Umebainika uhusiano mkubwa kati ya unywaji wa vinywaji baridi na vurugu, inawezekana ukawepo uhusiano wa moja kwa moja, labda kutokana na kiwango cha sukari na ‘kafeini’ kilichomo kwenye vinywaji hivyo au kunaweza kukawepo sababu nyingine ambazo hatukuzigundua kwenye utafiti wetu zinazo oanisha matumizi makubwa ya vinywaji baridi na tabia ya vurugu.

USHAURI
Watoto wetu hawezezi kujua vinywaji gani havina madhara kiafya kama mzazi hajawaambia na kuwaonesha kwa mfano kwa kutokunywa vinywaji hivyo. Kumfundisha mwanao vyakula na vinywaji vinavyokubalika kiafya ni jambo jema sana litakalomsaidia katika maisha yake yote na kamwe hawezi kupotoshwa na kampeni za matangazo.

2 comments:

Jacob'z Amigo Baraka said...
This comment has been removed by the author.
Jacob'z Amigo Baraka said...

mi naona sasa tutaanza kunywa maji...

Post a Comment

 
Design by Uplink Servers Technology | Bloggerized by Kwetu Bongo Online Magazine