
KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic, amesema iwapo itafikia hatua ya kutoelewana na kiungo Haruna Moshi ‘Boban’ (pichani), hatakuwa na msamaha naye.
Milovan, maarufu kama Profesa Chico, amesema taarifa za Boban kuondolewa kwenye timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, haijamshtua na hawezi kulichukulia suala hilo kama mfano mbaya kwa kiungo huyo kwa kuwa hajakorofishana naye.
Akizungumza na Championi Jumatano jana, Profesa Chico alisema atasubiri aanze kufanya kazi na Boban ili aweze kuangalia zaidi tabia yake lakini kama atafanya utovu wa nidhamu, basi atakalia benchi hata kama ana kipaji cha juu.
“Kosa alilomfanyia kocha wa timu ya taifa haliwezi kunifanya nimhukumu, wakati wa kufanya kazi na mimi ukifika, kila kitu kitajieleza. Sitakuwa na sababu ya kukumbuka ya nyuma, badala yake nitafanya kila kitu kwa kuangalia mimi na yeye (Boban) tunafanya nini.
“Suala la utovu wa nidhamu, sitalipa nafasi. Kingine nisisitize, yeye (Boban) hajakosana na mimi. Kwa kuwa ndiyo tunaanza msimu, nafasi ya kila mchezaji itakuwa sawa na inawezekana nikawa rafiki yake na tukashirikiana vizuri, hivyo tusubiri,” alisema Profesa Chico, aliyechukua nafasi ya Moses Basena wa Uganda.
Wiki iliyopita, Boban alitimuliwa kwenye kikosi cha Kilimanjaro Stars kutokana na utovu wa nidhamu, aliondoka kwenye benchi hata kabla ya mechi dhidi ya Zimbabwe kwisha.
Kocha Mkuu wa Kili Stars, Charles Boniface Mkwasa na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, walimwita Boban ikiwa ni baada ya kukosa nafasi wakati wa kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo na huyu wa sasa, Jan Poulsen, lakini hajatoa msaada mkubwa kwenye timu hiyo.
0 comments:
Post a Comment