Drogba akishangilia bao la kusawazisha |
Gomez akipiga mishemishe langoni mwa Chelsea |
Bayern wakishangilia bao la kuongoza |
Bao la Drgoba, Neur akichungulia mpira nyavuni |
MULLER AKIFUNGA BAO
CHELSEA
wametimiza ndoto za kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya
kuifunga Bayern Munich kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya
dakika 120, kwenye Uwanja wa Allianz Arena, Munich, Ujerumani.
Shujaa wa
Chelsea ni Didier Yves Drogba ambaye pamoja na kufunga penalti ya mwisho
ya ubingwa, pia alifunga bao la Chelsea ndani ya dakika 90. Lakini pia,
sifa zimuendee kipa Petr Cech aliyecheza penalti mbili za Bayern.
Wengine
waliofunga penalty za Chelsea ni David Luiz, Frank Lampard na Ashley
Cole, wakati Juan Mata yake iliokolewa Neur. Kwa upande wa Bayern,
waliofunga ni Lahm, Gomez na kipa Neur.
Lilikuwa bonge
la fainali na timu hizo zilimenyana vikali. Hadi mapumziko hakuna timu
iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake, Bayern wakitawala zaidi mchezo na
kupata kona kibao, lakini safu ya ulinzi ya Chelsea iliyoongozwa na
David Luiz ilikuwa imara kuwadhibiti The Bavarians.
Kipindi cha
pili Chelsea nao waliamua kuongeza kasi ya mashambulizi na kupata kona
tatu, lakini walikuwa ni Bayern Munich waliotangulia kuwainua vitini
mashabiki wao, dakika ya 83 kwa bao la Thomas Mueller, aliyeunganisha
kwa kichwa cha kudundisha chini krosi ya Toni Kroos na mlinda mlango wa
The Blues, Petr Cech akashindwa kuokoa.
Mara tu baada
ya bao hilo, Kocha wa Muda wa Chelsea, Roberto Di Matteo, alimuinua
mshambuliaji Fernando Torres kwenda kuchukua nafasi ya Solomon Kalou,
jambo ambalo liliongeza uhai wa safu ya ushambuliaji ya Blues.
Alikuwa ni
mshambuliaji ambaye anacheza mechi yake ya mwisho na jezi ya Chelsea,
Didier Yves Drogba aliyeisawazishia bao timu yake dakika ya 88, kwa
kichwa kikali akiunganisha kona iliyochongwa na Juan Mata.
Bao hilo
liliwanyamazisha malefu ya mashabiki wa Bavarians walioamini Mueller
kamaliza kazi na Kombe linabaki Munich- na tangu hapo timu hizo
zilishambuliana kwa zamu hadi kipyenga cha kuhitimisha dakika 90 na
mchezo kuhamia kwenye dakika 30 za nyogeza.
Katika dakika
ya tatu ya muda wa nyongeza, Drogba alimkwatua kwa nyuma kwenye eneo la
hatari Frank Ribery na refa akawapa penalti Bayern sambamba na kumpa
kadi ya njano mshambuliaji wa Ivory Coast.
Arjen Robben
alikwenda kupiga penalti dakika ya 94 na kipa Petr Cech aliyesema mapema
amekwishasoma hatua za wachezaji wa Bayern wakati wa upigani wa
penalti, alidhihirisha hilo kwa kupangua mkwaju wa winga huyo wa
kimataifa wa Uholanzi.
Cech ambaye
kesho anasherehekea miaka 30 ya kuzaliwa kwake, hakupangilia mbali mpira
huo, ilikuwa jirani mno na yeye na akaugeukia haraka na kuuficha kwenye
himaya yake.
Baada ya hapo,
timu hizo zilishambuliana kwa zamu na kwa tahadhari mno na hadi dakika
15 za kwanza zinamalizika ubao wa matokeo ulibaki kusomeka 1-1.
Dakika ya 107,
Daniel Van Buyten alipata nafasi nzuri akiwa anatazamana na kipa Cech,
lakini shuti lake la chini lilikwenda nje sentimita chache upande wa
kuliwa wa kipa huyo wa Chelsea. Huna sababu ya kutosema lilikuwa bao la
wazi walikosa Bayern.
Dakika ya 111
tena Bayern walifanya shambulizi kali langoni mwa Chelsea, lakini Luiz
akaokoa na kuna iliyokwenda kupigwa na Robben, lakini ikaondoshwa kwenye
hatari.
Dakika 120
zinatimu matokeo 1-1 na katika matuta, Chelsea wakafuta machungu ya 2008
walipofungwa na Manchester United kwenye fainali mijni Moscow.
0 comments:
Post a Comment