Waandaaji wa Miss Kigamboni 2012 Angela Msangi (kulia) na Somoe Ng'itu kushoto.
MAZOEZI kwa ajili ya kushiriki shindano la kumsaka malkia wa kitongoji cha Kigamboni
mwaka huu 'Miss Kigamboni City 2012' yameshaanza mapema wiki hii imefahamika.
Shindano hilo limepangwa kufanyika ifikapo Juni 15 kwenye
ukumbi wa Navy Beach ulioko huko Kigamboni hapa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana jijini, Mratibu wa shindano hilo, Somoe
Ng'itu, alisema kuwa maandalizi ya kinyang'anyiro hicho yanaendelea na warembo
tayari wameshaanza mazoezi kwenye ukumbi wa Break Point ulioko Posta jirani na
Club Billicanas.
Alisema kuwa bado milango iko wazi kwa warembo wenye sifa
kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini wanakaribishwa kushiriki kuwania taji
hilo.
Aliongeza kuwa kampuni yake imejipanga kuhakikisha shindano
la mwaka huu linakuwa bora na kuwapata washiriki watakaokwenda kutwaa taji la
Kanda ya Temeke na hatimaye taji la taifa la Redd's Miss Tanzania baadaye mwaka
huu.
"Kila kitu ni maandalizi, tumejiandaa katika kufanya
mchakato wa kupata warembo wenye sifa ili waweze kwenda kuiwakilisha vyema
Kigamboni katika mashindano ya Kanda," alisema Somoe.
Aliwataja warembo ambao wameshaanza mazoezi kuwa ni pamoja
na Caroline Peter, Theopisther Wenso, Sophia Martime, Amina Aboubakar, Aisha
Rajab, Rosemary Peter, Mariam Mbulilo, Julieth Phili na Doreen Kweka.
Warembo hao wanafanya mazoezi chini ya Hawa Ismail ambaye
alikuwa mshindi ya shindano la Kanda ya Temeke mwaka 2003.
"Bado tunakaribisha wadau wa sanaa ya urembo
kutudhamini shindano hili, tunaamini uwepo wao ndio utafanikisha ubora na hadhi
ya shindano letu mwaka huu kama tulivyodhamiria," aliongeza.
Aliwataja wadhamini ambao tayari wamethibitisha kudhamini
shindano hilo ni pamoja na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake
cha Redd's, Dodoma Wine na NSSF.
Taji la taifa la shindano hilo linashikiliwa na Salha Israel
ambaye alitokea katika Kanda ya Ilala.
0 comments:
Post a Comment