Monday, July 18, 2011

Wanachama TLP wamtaka Mrema aondoke

Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema

Upepo ndani ya Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) bado sio mzuri baada ya baadhi ya wanachama kutoa notisi ya kumtaka Mwenyekiti wa chama hicho Augustine Mrema kujiuzulu ndani ya siku tatu.
Kwa mujibu wa notisi hiyo iliyotolewa na mwanachama aliyejitaja kwa jina la James Haule, uamuzi huo umetokana na kutokubali uongozi huo kuendesha chama kwa katiba ya 2009.
Alisema, kwa ujumla wanachama wanatambua katiba halali inayoendesha chama hicho ni ya mwaka 1999 na sio vinginevyo.
“Mrema pamoja na viongozi wenzako mmekuwa mkifanya udanganyifu kwa kuendesha chama kwa kutumia katiba tofauti na matakwa ya katiba ya TLP ya mwaka 1999,” ilisema sehemu ya barua hiyo.
Ikaeleza kutokana na makosa hayo wanamuomba Mrema na viongozi wote kujiuzulu ndani ya siku tatu kuanzia jana kwa kuwa madaraka yao yapo kinyume na sheria ya nchi.
Aidha, Haule kwenye barua yake alisema kama muda huo ukipita na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa, hatua za kisheria ikiwa kulifikisha suala hilo Mahakamani litachukuliwa.
Hata hivyo, gazeti hili lilipowasiliana na Mrema kwa njia ya simu alisema hawezi kuhangaishwa na jambo hilo linaloonekana kuna mbinu ya kumchafua yeye na chama chake.
Alisema, mtu aliyesambaza barua hiyo hatambuliki ndani ya chama na hata madai yake yanaonekana kuwa watu wanamtumia ili kumdhoofisha.
“Katiba ya chama changu ni halali, hata ukienda kwa Msajili wa vyama anaitambua sasa anapoibuka mtu mmoja na kuipinga hilo naona sio jambo la maana, ni njaa tu hizo zinawasumbua,” alisema Mrema.
Aidha aliongeza kwamba kama kuna mtu ana wasiwasi na katiba hiyo aende katika ofisi Msajili au makao makuu ya TLP apate ufafanuzi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya Nje ya TLP, Stanley Temba alikiri kuiona barua hiyo, na kuielezea imeandikwa na walevi wa baa na hawezi kulizungumzia kwa undani.
“Mimi sikuletewa ofisini ila nimeona mitaani tu, naambiwa kwenye mabaa, barua vikaratasi hivyo vimesambazwa, sasa ikiwa zipo mpaka sehemu za ulevi naona si jambo la kulizungumza kiofisi,” alisema Temba. Aidha, alisema Haule huko nyuma alikuwa Mweka hazina wa vijana lakini alifukuzwa kutokana na kukiuka maadili na hivyo hawezi kuzungumzia suala lolote linalohusu TLP.

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Uplink Servers Technology | Bloggerized by Kwetu Bongo Online Magazine