Friday, April 6, 2012

Ugonjwa wa macho watua Azam na JKT






BALAA la ugonjwa wa macho wa Red Eyes, ambao umevamia jijini Dar es Salaam, umezikumba timu mbili za Ligi Kuu za Azam na JKT Ruvu.

Wachezaji nane wa timu hizo mbili inadaiwa wamekumbwa na ugonjwa huo, ambao huambukizwa kwa njia ya hewa tu.
Nyota wanne wa Azam FC wanaumwa na watatu kati yao walicheza mechi baada ya kupewa dawa wakati timu hiyo ilipoicharaza JKT Ruvu 4-1, juzi Jumapili.

Wachezaji wa Azam wanaoumwa ni pamoja na Kipre Tchetche, John Boko Adebayor, Abdulhalim Humoud 'Gaucho' na Ibrahim Mwaipopo. Kati yao, Tchetche, Humoud na Boko ndio walicheza mechi hiyo.

Daktari wa Azam, Paul Gomes aliliambia Mwanaspoti: Ugonjwa wa macho umetuvamia katika kambi yetu na kuwapata wachezaji wanne, Tchetche, Boko, Ibrahim na Humoud.

Hata hivyo, tumefanikiwa kuudhibiti kwa dawa na ndiyo maana kati yao hao, watatu wameweza kucheza mechi ya leo (juzi Jumapili), alisema Gomes. Nyota hao walicheza huku macho yao yakiwa na rangi nyekundu.

Tchetche alisema alicheza mchezo huo kwa kuwa alijisikia yuko fiti wakati Humoud alidai kuwa anaelekea kupona.
Katika hatua nyingine, JKT Ruvu nayo iliathirika kwani nyota wake wengi wa kikosi cha kwanza nao wamekumbwa na ugonjwa huo.

Nahodha wa JKT Ruvu, Shaibu Nayopa aliwataja nyota wa timu hiyo wanaoumwa macho ni pamoja na Mohamed Banka, George Minja, Hamis Msanza na Furaha Tembo.

Minja alikiri kuumwa ugonjwa huo na kudai unamtesa ingawa amesema hivi sasa anaendelea vizuri kidogo.

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Uplink Servers Technology | Bloggerized by Kwetu Bongo Online Magazine