skip to main |
skip to sidebar

5/16/2012 06:29:00 AM

Unknown
No comments

Timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) inatarajia kucheza mechi
nyingine ya kirafiki dhidi ya Afrika Kusini (Banyana Banyana)
itakayofanyika Mei 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Twiga Stars inayojiandaa kwa mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza
Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia imeingia tena
kambini jana (Mei 14 mwaka huu) kujiwinda kwa mechi hiyo itakayochezwa
Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa.
Banyana Banyana pia iko katika kinyang’anyiro cha kutafuta tiketi ya
Fainali za Nane za AWC ambapo katika raundi hii ya pili imepangiwa
Zambia na itaanzia mechi hiyo ugenini jijini Lusaka.
Mei 12 mwaka huu Twiga Stars ilicheza mechi ya kimataifa ya kujipima
nguvu dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors) iliyofanyika Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam. Kambi ya timu iko Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Ruvu
mkoani Pwani.
Naye Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa katika
kuimarisha kikosi chake kabla ya mechi ya Jumapili dhidi ya Banyana
Banyana amemwita tena kikosi mshambuliaji mkongwe Esther Chabruma.
Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua
waamuzi kutoka Rwanda kuchezesha mechi hiyo ya AWC kati ya Tanzania
(Twiga Stars) na Ethiopia.
Waamuzi hao ni Angelique Tuyishime atakayepuliza filimbi wakati waamuzi
wasaidizi ni Sandrine Murangwa, Speciose Nyinawabari na Salma
Mukansanga. Kamishna wa mchezo huo wa kwanza ni Catherine Adipo kutoka
Uganda.
Mechi ya marudiano itachezwa Dar es Salaam wiki mbili baadaye ambapo
mshindi atapata tiketi ya kucheza Fainali za Nane za AWC zitakazofanyika
Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
0 comments:
Post a Comment