Na Ezekiel Kamwaga, Khartoum
WAPINZANI wa Simba katika michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF), Al Ahly
Shendi ya Sudan, tayari wameanza visa.
Leo hii, wachezaji na viongozi wa Simba wametelekezwa kwa takribani
masaa matano hotelini na wenyeji hao ambao walikuwa wameahidi kuipeleka
Simba katika mji wa Shendi.
Wenyeji wa Simba nchini hapa ambao ni Shendi na Chama cha Mpira wa Miguu
Sudan (SFA), walikuwa wameahidi jana kwamba Wekundu wa Msimbazi
wataanza safari ya kwenda Shendi mara baada ya kupata kifungua kinywa
saa tatu asubuhi.
Hata hivyo, hadi kufikia saa nane mchana, hakukuwapo na basi lolote au
mwakilishi yeyote wa kutoka Shendi au SFA aliyekwenda kwenye Hoteli ya
Safiga ilikofikia Simba na kwa mujibu wa mawasiliano, walidai kwamba
wamekwama kwenye foleni.
Hali hiyo ilisababisha wachezaji na viongozi wa Simba kushinda nje ya
hoteli hiyo wakiwa wamekaa nje kwenye viti vichache, huku wengine wakiwa
wamesimama tu kwa muda wa zaidi ya masaa mawili hadi matatu kwa vile
muda wa kutoka hotelini ulikuwa umepita.
Kwa mujibu wa kanuni ya 14 (b) ya mashindano yanayosimamiwa na CAF, timu
yeyote inatarajiwa kusafirishwa kutoka eneo moja kwenda jingine katika
muda ambao unakubalika, labda kama imechelewa yenyewe.
Kuna umbali wa kilomita 150 kutoka mji mkuu wa Sudan, Khartoum iliko
Simba hadi mji wa Shendi na kama Simba itachelewa kuondoka jijini hapa,
maana yake ni kwamba itashindwa kufanya mazoezi leo jioni na hivyo
Shendi na SFA wamekiuka kanuni hiyo.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alieleza
kuchukizwa kwake na tukio hilo akisema linaonyesha namna Shendi na SFA
walivyojipanga kutumia mbinu za nje ya uwanja kushinda pambano hilo la
marudiano.
Katika pambano la kwanza lililofanyika jijini Dar es Salaam wiki mbili
zilizopita, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
“Sisi tulitaraji kukumbana na yote haya ambayo tunayaona sasa. Wanajua
kwamba hawataweza kuishinda Simba ndani ya uwanja na hivyo wameamua
kutumia mbinu chafu.
“Bahati nzuri, wachezaji wetu, benchi la ufundi na sisi viongozi
tumejiandaa kikamilifu kwa mambo kama haya. Hata hivyo, tutapeleka
mashitaka yetu kwa kamisaa wa mechi yetu kwa vile wao Shendi walipokuja
Dar tuliwahudumia vizuri kwa kila kitu,” alisema.
Kutokana na kuchelewa huko kuondoka, hoteli ya Safiga haikuwa imeandaa
chakula cha mchana kwa wachezaji na ilibidi Rage na daktari wa timu, Dk.
Cosmas Kapinga, waende kutafuta “vipoza njaa” kwa wachezaji wa Wekundu
wa Msimbazi.
Kwa upande wake, Dk. Kapinga alisema inachofanyiwa Simba ni kitu ambacho
kwa kitaalamu kinaitwa uchoshwaji wa kisaikolojia, lengo lake likiwa
kuiathiri timu kiakili.
“Katika mazingira kama haya, wachezaji na viongozi wanashindwa kufikiria
kuhusu mechi na badala yake wanafikiria kuhusu adha wanazozipata. Kama
watakuwa hawajaandaliwa vizuri kisaikolojia, hii inaweza kuwa mbaya. Kwa
bahati nzuri, wachezaji wa Simba wameandaliwa vizuri kwenye eneo hilo,”
alisema Kapinga.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment