By Besty Pius

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza bei mpya za aina zote za mafuta za jumla na rejareja zitakazoanza kutumika kuanzia leo, huku bei ya petroli ikishuka na bei za dizeli na mafuta ya taa zikipanda.
“Ewura inatangaza bei elekezi na bei kikomo za mafuta ya petroli hapa nchini. Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia Jumatatu, tarehe 5 Novemba 2011,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Haruna Masebu.
Alisema katika mabadiliko hayo, petroli imeshuka kwa Sh. 30.54 kwa lita sawa na asilimia 1.51; wakati bei ya dizeli imepanda kwa Sh. 40.74 kwa lita sawa na asilimia 2.00 na bei ya mafuta ya taa imepanda kwa Sh. 27.10 kwa lita sawa na asilimia 1.34.
Alisema mabadiliko hayo ya bei za mafuta nchini, yametokana na mabadiliko ya bei katika soko la dunia na kuimarika kidogo kwa thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani, sarafu ambayo hutumika katika manunuzi ya bidhaa za mafuta kwenye soko la dunia.
Alisema bei za jumla kwa kulinganisha matoleo hayo mawili, zimebadilika ambapo petroli imeshuka kwa Sh. 30.54 kwa lita sawa na asilimia 1.56, wakati bei ya dizeli imepanda kwa Sh. 40.74 kwa lita sawa na asilimia 2.07 na bei ya mafuta ya taa imepanda kwa Sh. 27.10 kwa lita, sawa na asilimia 1.39.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko.
Masebu alisema taarifa hizo zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.
Hata hivyo, alisema kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo kama ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na Ewura na ambayo ilichapwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 5 la Januari 9, mwak juzi na marekebisho yaliyofanywa kupitia Tangazo la Serikali Na. 216 la Julai 29, mwaka huu.
Alivitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.
Pia aliwashauri wateja kununua bidhaa za mafuta kutoka kwenye vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani.
0 comments:
Post a Comment