AZAM FC jana ilitumia vizuri uwanja wa nyumbani kuwafundisha soka wababe wa Simba, timu ya Villa Squad kwa kuitandika mabao 4-1 katika mechi ya Ligi Kuu bara kwenye Uwanja wa Chamazi. Villa ilikuwa ikijaribu kusaka ushindi wa tatu mfululizo baada ya awali kuitungua Simba bao 1-0, na kuipa kipigo cha mabao 2-1 Polisi Dodoma huku mabao yote yakifungwa na mshambuliaji Nsa Job. Jana mambo yalikuwa tofauti kwani walipelekwa puta na Azam na kushuhudia wakimaliza ngwe ya kwanza wakiwa nyuma kwa mabao 4-1. Mshambuliaji Job ambaye amekuwa akifunga mabao mfululizo kwa Villa, aliwashitua wenyeji kwa bao la mapema katika dakika ya 22 baada ya kumalizia nyavuni mpira wa kona uliochongwa na Ahmed Bin Salim. Bao la Villa lilikuja dakika moja baada ya Kipre Tchetche wa Azam kushindwa kutumia nafasi ya kubaki na kipa wa Villa, Daud Mwasonge kufunga bao baada ya kipiga shuti lililokosa 'afya' na kudakwa na kipa. Dakika sita baadaye Azam walijirekebisha na kusawazisha bao hilo kupitia kwa Salum Abubakar aliyefunga kwa shuti kali baada ya kuufuma mpira uliokolewa vibaya na mabeki wa Villa. Bao hilo liliwapa nguvu Azam, kwani dakika ya 28, kiungo aliyesajiliwa wakati wa dirisha dogo, Abdi Kassim alifunga bao la pili baada ya kumalizia vizuri krosi ya Ibrahim Shikanda. Dakika mbili kabla ya filimbi ya mapumziko Hamis Mcha aliipatia Azam bao la nne kwa shuti la karibu na lango, kabla ya sekunde chache baadaye Kipre kufunga bao la nne akimalizia pasi ya Hamis Mcha. Kipindi cha pili timu zote zilishambuliana kwa zamu huku Villa wakionekana kuja juu na kufanikiwa kupata bao la pili lililokataliwa na mwamuzi Judith Gamba kwa madai mfungaji Josep Maundi alikuwa ameotea. Kufuatia kukataa bao hilo, mwamuzi huyo alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya mashabiki kumrushia mawe na hivyo mchezo kulazimika kusimama kwa dakika kadhaa. Ushindi huo umeimaimarisha safari ya Azam kuzifukuza Simba na Yanga kileleni mwa msimamo baada ya kufikisha pointi 35 na kubaki katika nafasi ya tatu. Katika mechi nyingi, JKT Oljoro jana walipoteza mechi ya nne mfululizo baada ya kufungwa bao 1-0 Ruvu Shooting katika pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha. Bao pekee kwenye mchezo huo lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Mohamed Kijuso. Kagera Sugar imelazimishwa sare 2-2 na Moro United kwenye Uwanja wake wa Kaitaba na kupunguza hasira za mashabiki wake mjini Bukoba. Moro United ilikuwa ya kwanza kupata mabao kupitia mshambuliaji Andrew Kasembe aliyefunga kwa mpira wa adhabu baada ya Benedict Ngasa kufanyiwa faulo nje ya 18 na Charles Luhende. Ngasa alipatia Moro bao la pili akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Salum Kanoni, wenyeji Kagera Sugar waliamka na kusawazisha kupitia David Charles dakika 88 kabla ya kufunga la pili kwa penalti baada ya Gidion Sepo kushika mpira kwenye eneo la hatari. Aidha, kutoka Tanga wenyeji Coastal Union walitumia vizuri Uwanja wa Mkwakani na kuzoa pointi zote tatu baada ya kuibuka na ushindi wa bao 2-0 yote yakiwakwa wavuni na Daniel Lianga katika dakika ya 21 na 89. |
0 comments:
Post a Comment