|
KOCHA wa Yanga, Kosta Papic ameomba radhi kwa matokeo mabaya iliyopata timu yake kwa mchezo wa kwanza wa raundi ya awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri.
Katika mchezo huo ambayo Yanga imejiweka njia panda, inahitaji ushindi ama sare ya 2-2 iweze kusonga mbele. Kwa kanuni za mashindano hayo, endapo mechi hiyo itasimama suluhu, basi Yanga itakuwa imeaga michuano hiyo kwa kuwa Zamalek itakuwa na faida ya bao la ugenini.
Yanga iliyokosa mabao matano ya wazi, ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 36 lililofungwa na Hamisi Kiiza baada ya kupiga mpira wa mbali uliodhaniwa unatoka na kujaa wavuni.
Hata hivyo, Amr Zaki aliyeingia kipindi cha pili, aliisawazishia bao timu hiyo ambayo marudiano yake yatakuwa baada ya wiki mbili.
Papic alisema: Matokeo haya ni mabaya sana, naomba radhi mashabiki, viongozi na wale wote wapenzi wa Yanga, lakini nitakachofanya ni kuitengeneza safu ya ushambuliaji .
Tumetengeneza nafasi nyingi, lakini wachezaji wangu walikosa umakini na kushindwa kufunga...katika siku 10 za maandalizi ya mechi ya marudiano, naamini makosa yaliyojitokeza tutayarekebisha, nitakomalia washambuliaji, alisema Papic.
Papic ambaye alionekana kuchanganywa na kelele za mashabiki wa Simba kuwashangilia wapinzani wake, alisema kuwa atahakikisha anawashughulikia wachezaji wake kwa kuwa kazi kubwa ni kuwatoa Zamalek.
Hata hivyo, alisema kuwa nafuu yake ni Zamalek kucheza bila mashabiki, lakini pamoja na hayo alisema kukosa nafasi za kufunga kwa wachezaji wake kumewaweka katika mazingira magumu ya mchezo wa marudiano. |
|
0 comments:
Post a Comment