Saturday, March 3, 2012

YANGA YAPOTEZEWA NA MASHABIKI CAIRO

MECHI ya Yanga na Zamalek siyo gumzo sana mitaani katika jiji la Cairo, lakini kikosi cha wachezaji 20 cha Zamalek kipo kambini kikijinoa na tayari straika wao wa Benin, Razak Omotoyossi, ametua.

Ingawa timu hiyo itamkosa straika wake Amr Zaki ambaye ni majeruhi, lakini Ahmed Hossam Mido yuko fiti na kocha Hassan Shehata amemsifu kuwa yupo kwenye kiwango kizuri; Yupo kwenye fomu stahili.


Zamalek, ambayo imeweka kambi nje kabisa ya jiji la Cairo, Alhamisi ilifanyia mazoezi kwenye uwanja wake na jana Ijumaa ikafanyia katika uwanja mwingine mdogo ulioko nje ya jiji.


Mashabiki wanapoona basi la Yanga wala hawashtuki au kushangaa ingawa juzi Alhamisi jioni baadhi yao walidhani ni timu ya Taifa imekuja hapa kwa mchezo wa kirafiki na Misri.


Mmoja wa maofisa wa Tanzania jijini hapa alisema kuwa machafuko ya kisiasa yaliyotokea siku za karibuni, pamoja na kusimamishwa ligi kumewafanya mashabiki kutohangaika tena na soka la Misri.

Mechi ya Yanga na Zamalek hairuhusiwi kuwa na mashabiki kwa vile Zamalek imefungiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), jambo ambalo huenda likawaathiri ingawa juzi Alhamisi baadhi ya walinzi wa Uwanja wa Klabu walidai huenda ikawekwa idadi kubwa ya wanajeshi ambao watatumia kigezo cha ulinzi, lakini wataiweka Zamalek kwenye mazingira mazuri.


Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Chuo cha Jeshi la Misri nje kidogo ya jiji la Cairo kuanzia saa moja usiku kwa saa za Tanzania.

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Uplink Servers Technology | Bloggerized by Kwetu Bongo Online Magazine