Wednesday, May 23, 2012

SIMBA YAMSAJILI MUDDE



KIUNGO wa Uganda, Mudde Mussa, ambaye amesajiliwa na Simba amedai kuwa anaamini timu yake mpya itamsaidia kutimiza ndoto yake ya kucheza soka Ulaya.

Mudde, ambaye amesajiliwa kutoka Sofapaka ya Kenya, aliiambia Mwanaspoti kuwa ataitumia fursa ya kuchezea Simba vizuri ili apige hatua kisoka.

"Ni kweli kabisa nimesaini kuichezea Simba kwa mkataba wa miaka miwili, siku zote huwa sipendi kurudi nyuma hivyo nataka Simba ndio iwe tiketi yangu ya kwenda Ulaya.

"Nikuambie jambo moja, unapotaka mafanikio wakati mwingine hutakiwi kuangalia fedha tu, Simba inashiriki michuano mikubwa mara nyingi, hiyo ni sehemu nzuri ya mtu mwenye malengo kuweza kufikia matarajio,"alisema Mudde.

Musa alisema kuwa ili kuonyesha kwamba hakusajiliwa kimakosa atahakikisha anaisaidia Simba kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Kagame itakayofanyika baadaye mwezi hujao.

"Kwa sasa nipo timu ya taifa tunajiandaa na mechi dhidi ya Angola Juni 3 , lakini nawaambia Watu wa Simba wasiwe na hofu Mungu akipenda wataniona Kagame kwani nimepania kuthibitisha thamani yangu,"alisema kiungo huyo mkabaji.

Naye nyota wa zamani wa Simba, Patrick Ochan amesema Simba wamelamba dume kwa Mudde kwani atawasaidia kwenye michuano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Ochan ambaye anaichezea klabu ya TP Mazembe ya Congo, alisema Mudde ni kati ya wachezaji bora wa kiungo kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

"Mudde anacheza nafasi nyingi na atawasaidia sana kwenye michuano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi na mashabiki wa Simba watarajie mambo makubwa kwenye timu," alisema Ochan, ambaye yuko TP Mazembe akiwa na wachezaji wa Tanzania, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu.

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Uplink Servers Technology | Bloggerized by Kwetu Bongo Online Magazine