Na Mwandishi Wetu
NAHODHA wa Klabu ya FC Leopards ya Kenya, Salim
Kinje, anajiandaa kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba kwa
ada ya zaidi ya Sh milioni 90.
Kiungo huyo ambaye ni raia wa Tanzania, anatua Simba baada ya
kuwindwa kwa muda mrefu na timu iliyoshika nafasi ya pili kwenye ligi kuu msimu
uliopita, Azam FC.
Mtandao wa SuperSport.com umesema kuwa mchezaji huyo ambaye
amezivutia klabu nyingi za Tanzania,
ataondoka na kujiunga na Simba kwenye usajili wa mwezi ujao.
Imefahamika kuwa sababu kubwa ya mchezaji huyo kujiunga na
Simba ni kuweza kupata nafasi ya kukichezea kikosi cha timu ya taifa, Taifa
Stars.
Kocha wa Leopards, Jan Koops, amethibitisha kuondoka kwa
mchezaji huyo na kusema hataendelea tena kuitumikia timu hiyo.
“Kinje aliniita na kuniambia kuwa amepata ofa nzuri kwenye
kikosi cha Simba na anataka kuondoka. Huyu ni Mtanzania na anataka kwenda
kucheza soka nchini kwao.
“Tutammisi sana, alikuwa kiongozi mzuri wa wachezaji wetu,
alikuwa nahodha wa pili wa timu na hili ni pigo kubwa sana kumpoteza.”
Taarifa kutoka kwenye Mtandao wa Ingwefans wa Kenya,
zinasema kuwa Simba inamsajili kiungo huyo kwa kitita cha shilingi za Kenya
milioni 5 ambazo ni zaidi ya shilingi za Kitanzania milioni 90.
Mtandao huo umeendelea kueleza kuwa kiungo huyo anatarajiwa
kutoka Kenya leo ili kuja kukamilisha mkataba na Wekundu hao baada ya kuwaaga
wachezaji wenzake juzi.
Maoni ya mashabiki wa timu hiyo kwenye mtandao huo yalionyesha
kuwa Kinje alikuwa mmoja wa wachezaji tegemeo kabisa wa kikosi hicho lakini
wengi waliamini kuwa kitita cha fedha kilichotolewa na Simba kitaweza
kuibadilisha timu hiyo.
Akizungumzia suala hilo, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel
Kamwaga, alishindwa kukubali au kukataa. Alisema: “Tunajua kwamba Kinje ni
mchezaji mzuri lakini kwa sasa hatuwezi kusema kama tutamsajili au
hatutamsajili.”
CHANZO:GAZETI LA CHAMPION
CHANZO:GAZETI LA CHAMPION
0 comments:
Post a Comment