Monday, July 30, 2012

Mwakyembe aapa kulifufua Shirika la Ndege ATCL



 

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amewataka Watanzania kumpa miezi mitatu kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili liweze kufanyakazi kwa umakini na kutoa ushindani katika usafiri wa anga.
Akizungumza  juzi jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa karakana ya Shirika la ndege la Precision Air, alisema amepania kulirudisha shirika hilo kwenye uhai kwa kuwa ni tegemeo kubwa kwa maslahi ya nchi na Watanzania.
Alisema shirika hilo ni mkombozi pekee katika usafiri wa anga kwa Watanzania na kwamba nia ya serikali ni kuhakikisha linafanyakazi kwa kujiendesha na gharama za usafiri huo ziwe nafuu.
“Nimeona wananchi wataumia tukiiondoa ATCL kwa sasa suala hili ninaliangalia, nipeni miezi mitatu shirika hilo litarudi na kufanya shughuli zake kwa umakini,” alisema.
Alisema hali ya usafiri wa anga Tanzania inatakiwa kuboreshwa ili kuwepo na ushindani na mashirika ya ndege ya nchi zingine kwa lengo la kuongeza uchumi wa nchi.
Akizungumzia suala la mikataba mibovu iliyoko katika sekta yake alisema kwa sasa anachokifanya ni kuipitia na kuitolea ufafanuzi hivi karibuni kwani amegundua kuwepo kwa madudu mengi katika suala hilo.
Dk. Mwakyembe alisema kuwepo kwa mikataba mibovu kunasababisha kutokuwepo kwa utendaji mzuri wa kazi na kwamba katika suala hilo hatakubali kuona wizara yake ikiingia katika mikataba mibovu. Shirika hilo limekuwa likijiendesha kwa kusuasua kiasi cha kusababisha makampuni ya ndege binafsi kuteka sekta hiyo ya usafiri wa anga nchini.
Shirika ambalo kwa sasa linatamba nchini kwa usafiri wa anga ni la Precision Air ambalo limeweza kupasua anga si nchini bali hata nchi za nje.
ATCL ambayo imekuwa ikijikongoja kwa ndege yake moja na baadaye kukaa juu ya mawe, ilianza tena safari zake za ndani miezi michache iliyopita na kuanza kuleta matumaini kwa wasafiri wanaotumia usafiri huo wa anga.
Katika siku za karibuni Waziri Mwakyembe, alibadili safu ya uongozi wa shirika hilo baada ya kubaini kuwa kulikuwepo na ukiukwaji wa sheria ya uajiri.
Tangu ahamishiwe wizara ya uchukuzi, Waziri Mwakyembe amekuwa akitembelea mashirika ya usafiri kujionea changamoto zinazozikabili mashirika hayo.

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Uplink Servers Technology | Bloggerized by Kwetu Bongo Online Magazine