Monday, August 13, 2012

CHAMA CHA KIJAMII(CCJ) KIMEIBUKA NA MBINU MPYA


Chama Cha Kijamii (CCK) kimeibuka na kuishukia Serikali kwa kushindwa kutimiza wajibu wake kwa wananchi na kufanya kuibuka migomo kwa kada mbalimbali wakiwemo madaktari na walimu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi, serikali inatakiwa kutimiza wajibu wake kwa kufanya mazungumzo kwa kile walimu na madaktari wanachodai ili kuepusha migomo ya mara kwa mara.
Alisema serikali inatakiwa  kujua kuwa migomo si harusi wala sherehe, bali ni lugha ya watu ambao wanahisi hawasikilizwi na historia hiyo ya migomo inatakiwa iangaliwe upya.
Alisema serikali ya nchi ya demokrasia haingii madarakani kwa amri ya mahakama bali kwa kuzungumza na wananchi wake kwa kuwashawishi wawape madaraka hivyo wananchi wanapokuwa na swali, serikali inatakiwa kutumia njia hiyo ya mazungumzo ili wananchi wake waridhike.
“Serikali itambue kuwa madaktari na walimu kwa pamoja wanapeleka ujumbe wa dhati na wa kweli kwa kuwa mishahara yao haitoshi na wao siyo wanasiasa,” alisema Muabhi.
Akizungumzia mgogoro wa  Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi, alisema kauli za viongozi zimekuwa za kushabikia vita badala ya kutafuta njia mbadala ya mazungumzo ili kutatua mgogoro.

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Uplink Servers Technology | Bloggerized by Kwetu Bongo Online Magazine