Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa akiwasilisha hotuba
ya makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2012/13
Bungeni,Dodoma, jana.
SERIKALI
imetenga Sh326 bilioni kwa ajili ya kugharimia mikopo ya elimu ya juu
kwa wanafunzi 98,772 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/13.Idadi
hiyo ya wanafunzi ni ongezeko la takriban wanafunzi 5,596 ikilinganishwa
na wanafunzi 93,176 waliopata ufadhili wa bodi hiyo mwaka jana.
Hayo
yalielezwa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru
Kawambwa wakati akisoma Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara yake
kwa mwaka wa fedha 2012/13.
“Katika mwaka 2012/13, wizara kupitia
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, itatekeleza yafuatayo;
kutoa mikopo kwa wanafunzi 98,772 wa vyuo vya elimu ya juu na kusimamia
ukusanyaji wa marejesho ya mikopo ya Sh18 bilioni kwa kuchukua hatua za
kisheria dhidi ya wadaiwa,’’ alisema Dk Kawambwa.
Waziri alisema
kati ya wanafunzi 93,176 waliopata mikopo kwa kipindi cha mwaka wa fedha
uliopita, 256 walikuwa wahadhiri ambao walikuwa wakisomea shahada za
uzamili na uzamivu ndani na nje ya Nchi.
Alisema katika mwaka huu wa
fedha, Wizara inakusudia kudahili wanafunzi 65,000 wanaojiunga na vyuo
vikuu kama hatua za kufikia lengo la wanafunzi 300,000 kwenye Taasisi ya
Elimu ya Juu ifikapo mwaka 2015.
Alisema mipango mingine ni
kuanza mchakato wa ujenzi wa ofisi za bodi ili kuongeza ufanisi katika
kazi na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu wajibu wa
kuchangia elimu ya juu na urejeshaji wa mikopo.
Waziri
alisema Wizara yake inaendelea kuongeza ufanisi katika usambazaji wa
mitihani kwa kununua matrela mawili ya malori na magari madogo mawili
kwa ajili ya ufuatiliaji na usindikizaji wa mitihani hiyo.
Alisema
kupitia Baraza la Mitihani la Taifa, Wizara itasimamia Mtihani wa
Kumaliza Elimu ya Msingi kwa watahiniwa 1,050,000 wanaotarajia kufanya
mtihani huo mwaka huu.
Katika bajeti hiyo, Waziri Kawambwa aliomba
Bunge liidhinishe matumizi ya Sh724.5 bilioni kwenye wizara hiyo kwa
mwaka huu wa fedha ikiwamo ni fedha za matumizi ya kawaida, mishahara na
matumizi mengineyo.
Kamati: Kodi zipitiwe upya
Serikali
imeshauriwa kupitia upya utaratibu wa kodi zinazotozwa kwa taasisi
binafsi za elimu nchini zikiwamo zinazotoa elimu ya msingi na sekondari
ili kuzisaidia taasisi hizo kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu.
Ushauri
huo ulitolewa bungeni jana na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Martha
Mlata wakati akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma
za Jamii kuhusu Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa
mwaka 2012/13.
Mlata alisema watu na taasisi binafsi za elimu
nchini zimekuwa zikichangia juhudi za Serikali katika kutoa elimu ya
msingi, sekondari na vyuo kwa kuzingatia miongozo ya wizara lakini
zinakabiliwa na changamoto kubwa ya kodi.
“Taasisi hizi
zinakabiliwa na changamoto ya utozwaji wa kodi ikiwamo kodi za ardhi,
majengo, mapato, kodi ya kuajiri mwalimu au mfanyakazi asiye raia wa
Tanzania hali inayosababisha uendeshaji wa taasisi kuwa mgumu,” alisema.
Kamati
hiyo pia imebainisha kuwapo kwa mgongano katika utekelezaji wa sera ya
uchangiaji elimu hususan utoaji wa elimu ya msingi na sekondari hali
inayosababisha baadhi ya wazazi kugoma kuchangia elimu kwa watoto wao.
Madai ya Upinzani
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeitaka Serikali kuwarudisha vyuoni
wanafunzi 285 wa vyuo vikuu waliosimamishwa masomo wakigomea utendaji
mbovu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi Nchini.
Msimamo huo
uliwasilishwa bungeni jana na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan
Lyimo wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu Bajeti ya Wizara ya
Elimu na Mafunzo 2012/13.
Kati ya wanafunzi hao, 260 ni wa Chuo Kikuu Dodoma (Udom) na wanafunzi 25 ni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
0 comments:
Post a Comment