Abdallah Zombe
JAJI
wa Mahakama ya Rufani, Semistocles Kaijage amekwamisha usikilizwaji wa
rufaa ya Serikali dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es
Salaam (RCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na
wenzake wanane, baada ya kuugua.
Serikali
kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ilikata rufaa kupinga hukumu ya
Mahakama Kuu iliyowaachia huru Zombe na wenzake katika kesi ya mauaji ya
wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na
dereva wa teksi wa Manzese jijini Dar es Salaam.
Rufaa
hiyo ilitarajiwa kusikilizwa jana na Jopo la Majaji watatu wa Mahakama
ya Rufani, lakini ilishindikana kutokana na kuugua kwa Jaji Kaijage
ambaye ni mmoja wa majaji katika jopo hilo, na kulazimika kuahirishwa.
Mbali
na Jaji Kaijage, ambaye amechukua nafasi ya Jaji William Mandia
aliyekuwa mmoja wa majaji katika jopo la awali, majaji wengine katika
jopo hilo ni Nathalia Kimaro, ambaye ndiye kiongozi wa jopo na Katherine
Oriyo.
Taarifa
za kuugua kwa Jaji Kaijage zilitolewa na Jaji Kimaro kwa pande zote
katika rufaa hiyo, wakati akiahirisha usikilizwaji wa rufaa hiyo.
Akiahirisha
usikilizwaji wa rufaa hiyo, Jaji Kimaro alisema kuwa rufaa hiyo
itasikilizwa kwa tarehe nyingine itakayopangwa na msajili na kwamba
wadaiwa wote watajulishwa, tarehe hiyo mpya itakapokuwa imepangwa.
Katika
kile kilichoonekana kuwa ni kujizatiti zaidi, jana upande wa mrufani
(Jamhuri) ulikuwa na jumla ya mawakili saba na upande wa wajibu rufaa
ulikuwa na jumla ya mawakili watano.
Jopo
la mawakili wa Serikali liliongozwa na Wakili wa Kujitegemea, kutoka
mkoani Tabora, Mutaki akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi,
Angaza Mwipopo ambao wote waliendesha kesi ya msingi.
Wengine
ni Alexander Mzikila, ambaye pia alikuwa ni mmoja wa mawakili wa
Serikali walioendesha kesi ya msingi, lakini kwa sasa ni wakili wa
kujitegemea.
Mbali
na mawakili hao waliokuwepo kwenye kesi ya msingi, jana Serikali
iliongeza nguvu kwa kuongeza mawakili wengine wanne ambao ni Timon
Vitalis, Edwin Kakolaki, Prudence Rweyongeza, wote wakiwa ni Mawakili wa
Serikali Wakuu na Peter Njike, Wakili wa Serikali Mwandamizi.
Jopo
la mawakili wa wajibu rufaa liliongozwa na Wakili Richard Rweyongeza,
anayemtetea mrufaniwa wa kwanza, (Zombe), Gaudioz Ishengoma, kwa mrufani
wa pili, Christopher Bageni, Majura Magafu kwa warufani wa Denis
Msafiri.
Zombe
na wenzake walikuwa wakidaiwa kuwaua kwa makusudi wafanyabiashara hao
Sabinus Chigumbi, maarufu kwa jina la Jongo na ndugu yake Ephrahim
Chigumbi, Mathias Lunkombe pamoja na Juma Ndugu, dereva teksi.
Walikuwa
wakidaiwa kutenda kosa hilo Januari 14, 2006, katika msitu wa Pande
uliopo Mbezi Luis, Jijini Dar es Salaam, baada ya kuwatia mbaroni eneo
la Sinza Palestina na kuondoka nao wakiwa hai wakiwatuhumu kuwa ni
majambazi.Hata hivyo, Septemba 17, 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam iliwaachia huru washtakiwa wote ikisema kuwa baada ya kusikiliza
ushahidi na hoja za mawakili wa pande zote imeridhika kuwa washtakiwa
hawakuwa na hatia ya mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.
Jaji
Salum Massati (sasa Jaji wa Mahakama ya Rufani), aliyekuwa akisikiliza
kesi hiyo alisema kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha
mashtaka dhidi ya washtakiwa hapo bila kuacha mashaka.
Hata
hivyo siku chache baada ya kuachiwa huru, DPP alikata rufaa Mahakama ya
Rufani, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu, akidai kuwa Jaji Massati
alikosea kuwaachia huru washtakiwa hao.
DPP
katika rufaa hiyo namba 254/2009, iliyofunguliwa Oktoba 6, 2009,
amebainisha sababu 11 ambazo zimemfanya apinge hukumu hiyo yote, akidai
kwamba kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, washtakiwa wote
walikuwa na hatia.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment