KAMATI ya Mazishi ya aliyekuwa Msanii
wa Bongo Fleva, Albert Mangwea ‘Ngwea’, mpaka jana mchana ilikuwa
imekusanya jumla ya Sh milioni 32 kutoka kwa wadau mbalimbali.
Kamati hiyo inahitaji Sh milioni 50
kwa ajili ya kusaidia kusafirisha mwili wa marehemu kutoka Afrika Kusini
mpaka Morogoro kwa ajili ya mazishi. Fedha hizo pia zinahitajika kwa
ajili ya kuratibu shughuli nzima ya mazishi.
Mangwea alifariki dunia Jumanne
iliyopita nchini Afrika Kusini akiwa usingizini kwa madai ya kuzidisha
matumizi ya madawa ya kulevya.
Alitarajiwa kuwasili nchini jana
lakini kushindwa kutoka kwa ripoti ya uchunguzi wa madaktari kwa wakati,
kumesababisha isijulikane atatua lini, licha ya kudaiwa kuwa anaweza
kutua leo.
Kamati ya Mazishi bado inaendelea na mchakato wa kuratibu shughuli hiyo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mwandishi wetu akiwa
Mbezi Goig jijini Dar ambako ndiko kwenye msiba huo, mmoja wa waweka
hazina wa kamati hiyo, Paul Matthysse ‘P-Funk’, alisema mpaka sasa
kamati yake imefikisha Sh 32,259,000 ingawa wanatarajia kuendelea
kupokea michango mbalimbali kutoka kwa wadau.
Miongoni mwa watu wa kwanza kutoa
michango yao katika msiba huo ni P-Funk aliyetoa Sh milioni tano, Clouds
Media Group (Sh milioni tano) na Push Mobile (Sh milioni tano).
Juzi Kampuni ya Global Publishers ilitoa Sh milioni moja.
“Nawasisitiza Watanzania waendelee
kutoa michango yao kwa ndugu yao ili kuonyesha umoja tulionao. Fedha
zikiwa nyingi tunataka kumfanyia kitu mama yake ili kuendelea kumfariji
kwani kipindi hiki ni kigumu kwake,” alisema P-Funk.
Wakati huohuo jana taarifa zilisema
mama mzazi wa Mangwea aishie Morogoro, Denisia Mangwea, alipandwa na
presha baada ya jana kupata taarifa kuwa mwili wa mwanaye umezuiwa
Afrika Kusini kutokana na uchunguzi wa madawa ya kulevya. Alikimbizwa
hospitali na inadaiwa anaendelea vizuri.
Mangwea aliwahi kutamba na nyimbo kadhaa kali zikiwemo Gheto Langu, She Got a Gwan, Mikasi na Tupo Juu.
0 comments:
Post a Comment