Friday, September 6, 2013

Bungeni September 5 2013 Wabunge kutolewa na askari


BUNGENI 
Kwa mara nyingine tena vurugu zimezuka ndani ya ukumbi wa Bunge Dodoma 104.4 September 5 2013 baada ya Naibu Spika wa BUNGE JOB NDUGAI kuamuru askari wa Bunge kuingia ndani ya Ukumbi na kumtoa Kiongozi wa kambi ya Upinzani bungeni FREEMAN MBOWE kutokana na kukaidi agizo la kukaa chini lililotolewa na Naibu Spika wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Unaambiwa kabla ya vurugu zilizodumu kwa zaidi ya Dakika 15 kutokea na kusababisha kusimama kwa muda wa shughuli za Bunge, Mbunge wa Mkoani ALI KHAMIS SEIF aliomba muongozo wa Spika na kutaka kuahirishwa kwa muswada huo hadi Kamati ya Bunge ya Katiba, itakapopata fursa ya kwenda Zanzibar kupata maoni.

Alisema ‘kamati inayohusika na katiba, sheria na utawala haikwenda Zanzibar, mimi ni mjumbe wa kamati hiyo…  ilikua na utashi wa kwenda, nataka bunge liahirishe mjadala huu ili kamati iende Zanzibar na mjadala huu uahirishwe mpaka bunge la 13′

Pamoja na vurugu hizo kwa mara ya kwanza katika historia ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge wamelazimika kupiga kura ya mmoja mmoja kwa sauti kama inavyofanyika wakati wa kupitisha Bajeti ya Serikali ili kukubali au kukataa kuendelea kwa mjadala huo na matokeo yalikuwa hivi.

Jumla ya wabunge wote ni 351, ambao hawakuwepo bungeni ni 136, katika kura zilizopigwa za ndio ni 59, 156 zimesema sio.

Matokeo hayo hayakumridhisha kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni Freeman Mbowe ambae aliomba nafasi ya kuzungumza lakini hakuipata ambapo ndio zengwe lilitokea mpaka askari kuja kumchukua Mbowe na kumpeleka nje akiambatana na wabunge wengine wa upinzani.

Awali wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu MIZENGO PINDA, amesema Serikali haiwezi kuuondoa bungeni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kutokana na kuzingatiwa kwa hatua zote zinazopaswa kupitiwa wakati wa maandalizi ya Muswada wa sheria, ikiwemo kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali.

Akijibu swali la Kiongozi ya Kambi ya Upinzani bungeni FREEMAN MBOWE, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu PINDA amesema nafasi iliyopo ni nzuri kwa wabunge wote kuujadili muswada huo, na kubadili vipengele wasivyoridhika navyo, kabla ya kuupitisha.

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Uplink Servers Technology | Bloggerized by Kwetu Bongo Online Magazine