Friday, July 15, 2011

MAN CITY YAFANIKIWA KUMNASA GAEL CLICHY..



MANCHESTER, England

KLABU ya Manchester City imesema imemsajili beki wa kushoto wa Arsenal, Gael Clichy kwa pauni 7 milioni, lakini hawajaweka wazi wamesamjili kwa kiasi gani mchezaji huyo kwa msimu 2011/2012.

Clichy ambaye ni beki wa kimataifa wa Ufaransa alikuwa akihusishwa kuhamia klabu ya Manchester City wiki chache zilizopita, lakini hivi sasa ametua katika klabu hiyo kwa mkataba wa miaka minne.

Clichy,25, ameichezea Arsenal mechi 264 zikiwepo mechi 41 za Ligi ya Mabingwa barani Ulaya na amekuwa mchezaji wa nne wa Arsenal kuhamia klabu ya Manchester City.

Akiongea katika mtandao wa Manchester City, Clichy alisema,"Nina furaha kujiunga na klabu bora ya Manchester City, nina matumaini nitacheza kwa kiwango cha juu na kutoa mchango wangu katika kikosi cha Manchester ambacho kinao tayari wachezaji bora, tunacho kikosi bora ambacho ninaamini kitaendelea kuwa kizuri."

"Ninasubiri kwa hamu kuanza kucheza soka katika kikosi cha Manchester City na ninafikiri kila kitu kitawezekana katika klabu hii, nina maelewano na wachezaji wengi wa Manchester City, Kolo Toure alikuwa akinichukua na kunipeleka nyumbani pia mke wake walikuwa akipika chakula na sisi kula, Patrick Viera alikuwa siku zote akinipa ushauri kwa hiyo ni vizuri kwangu kuwa tena na wachezaji hawa,"alisema Clichy.

Clichy ametumia miaka nane akiwa chini ya kocha wa Arsenal, Arsene Wenger na kuondoka kwake ni uhamisho mkubwa katika kipindi hiki cha usajili nchini England.

Clichy alisema,"Nilikuwa na miaka nane mizuri katika klabu ya Arsenal na kupata marafiki wengi, nina kumbukumbu nyingi za Highbury na uwanja wa Emirates, ninapenda kusema asante kwa kila mtu katika klabu ya Arsenal kwa ushirikiano walionipa na urafiki wao, vilevile ninapenda kuwashukuru mashabiki wote wa Arsenal kwa sababu walikuwa ni watu wazuri kwangu."

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger ameupa baraka uhamisho huo na aliandika ujumbe kwenye mtandao wa klabu ya Arsenal akionyesha anaunga mkono uhamisho huo.

Wenger alisema,"Tunapenda kumshukuru Gael kwa miaka nane muhimu katika klabu ya Arsenal alitoa mchango mkubwa, aljitoa sana kuitumikia klabu ya Arsenal, amekulia na kuongeza uwezo wake wa kutandaza soka katika klabu ya Arsenal tangu alipojiunga na klabu ya Arsenal akitokea klabu ya Cannes ya Ufaransa na amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha kwanza cha Arsenal katika misimu ya hivi karibuni, Gael anaondoka kwa heshima zetu zote na tunamtakia mafanikio mema, tunamtakia maisha mema na bora katika uchezaji wake wa soka.

"

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Uplink Servers Technology | Bloggerized by Kwetu Bongo Online Magazine