Che Mundugwao akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa BSS kwa mwaka
2011 Hadj Ramadhan (Kushoto) na Waziri Salum.
Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii waliotoka katika
programu ya kusaka vipaji vya muziki ya Bongo Star Search kuwa na
mikakati ya kujiendeleza wenyewe ili kufikia kilele cha mafanikio.
Wito huo ulitolewa jana na mratibu wa BSS kutoka BASATA Vicky Temu
wakati akichangia katika kikao cha tathimini ya shindano hilo
kilichofanyika Ukumbi wa BASATA mapema wiki hii.
Vicky alisema kuwa, wasanii hao wanatakiwa kutambua kuwa uhusiano kati
yao na shindano la BSS unalindwa na kusimamiwa na mikataba wanayotiliana
saini toka wanapoingia kwenye shindano hilo hivyo inapofikia ukomo
hawana budi kujipanga kwa ajili ya kujiendeleza kisanaa.
“Wasanii wanaoshiriki BSS wanapaswa kuwa na mikakati ya kujiendeleza
baada kuwa wametambuliwa.Shindano hili linawaibua kutoka chini hivyo
lazima kuwe na daraja linalowafanya wajiendeleze kisanaa” alisisitiza
Bi. Temu.
Hata hivyo, wadau waliochangia kwenye tathimini hiyo walimtaka mwandaaji
wa shindano hilo Ritha Paulsen kuangalia namna ya kujenga daraja la
kuendeleza vipaji vinavyokuwa vimepatikana kwani wengi wao wanatoka
mikoani na hivyo kukosa mbinu za kuingia kwenye soko la muziki.
Walimshauri awe na utaratibu wa kuwaandalia semina na kozi fupifupi
washiriki wa shindano hilo zitakazolenga kuwaandaa kuingia kwenye soko
la muziki lakini pia kuwa wajasiliamali wazuri katika Sanaa.
“Washiriki wa BSS wanapokuwa kwenye kambi waandaliwe vema kuingia
kwenye soko la muziki. Wengi wao wanakosa mbinu na mikakati ya kuliteka
soko kutokana na kutoka mikoani hivyo wasaidiwe na wapewe mafunzo au
elimu katika eneo hili” alishauri Mjumbe.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Matukio kutoka BASATA, Malimi
Mashili aliwataka waandaaji wa BSS kuhakikisha wanatekeleza maagizo
mbalimbali waliyopewa kwa ajili ya kupatiwa kibali cha kuendesha
shindano hilo mwaka huu.
Maagizo waliyopewa waandaaji hao ni pamoja na; kuwa na bajeti kamili ya
shindano hilo, kuwekwa wazi kwa zawadi za washindi, kuwepo kwa mikataba
baina ya washiriki na BSS, kuwasilisha majina ya majaji wa shindano
hilo, uwezo wa BSS kuendesha shindano hilo na maagizo mengine.
Akizungumza kwenye tathimini hiyo, Mwandaaji wa shindano hilo Ritha
Paulsen alisema kuwa, shindano hilo limekuwa likimgharimu fedha nyingi
lakini kwa kuwa limejikita kwenye kuinua vipaji vya wasanii wachanga na
anapenda kusaidia analazimika kufanya.
“Shindano hili tunalifanya kwa gharama kubwa sana lakini tunajitahidi
kusaidia wasanii wetu ili wafahamike na baadaye wajisimamie katika kazi
zao” alisisitiza Ritha.
Aliongeza kuwa, BSS imekuwa ikijitahidi kusaidia wasanii katika kurekodi
na kujiendeleza lakini changamoto kubwa imekuwa kwa vyombo vya habari
na wakuzaji sanaa (mapromota) kuwapokea wasanii hawa kutokana na
kukithiri kwa vitendo vya rushwa na mtizamo hasi kuwa, wasanii wanaotoka
BSS wanakuwa na fedha nyingi.
Kuhusu maagizo aliyopewa na BASATA aliahidi kuyafanyia kazi ilil kupewa
kibali cha mwaka huu kwa ajili ya mchakato wa shindano hilo kuanza
mapema wiki hii.
0 comments:
Post a Comment