Monday, February 6, 2012

CHOKI KAVUNJA UKIMYA



ALLY Choki, ambaye ni kiongozi wa bendi ya Extra Bongo inayofanya vizuri Bongo, amesema kuwa wasanii wa Jamhuri ya DR Congo waliopo Tanzania wamepoteza dira katika muziki.

Mwanamuziki huyo ambaye hakumumunya maneno, amesema wasanii hao hawana jipya ndiyo maana bendi zao zimeanza kushuka baada ya watu kuelewa ukweli wa mambo.

Kwa maoni yangu hizi bendi za Wakongo zilizopo hapa Bongo hazina jipya, zimepoteza dira ndiyo maana huwezi kusikia kitu kipya au zikitamba kama ilivyokuwa siku za nyuma,alisema Choki.

Walikuwa wanadanganya watu sana kipindi cha nyuma lakini sasa watu wamekuwa wajanja, kuna kazi za wenzao walikuwa wanaiga wakajua kwamba hatutajua, lakini tumejua kutokana na utandawazi.

Mimi nimekwenda Kinshasa hivi karibuni, sijaenda kuiga kazi za bendi za kule au kumchukua mtu. Nimekwenda kujifunza kuangalia wenzetu wanafanya nini na mimi ninaweza kujifunza nini kutoka kwao niendeleze kazi yangu. Ndivyo binadamu tunavyofanya.

Lakini siyo kuiga sebene la Wenge halafu unawadanganya watu kwamba ni ubunifu wako, mashabiki ni wajanja sana siku hizi.

Huu ni mwaka wa bendi za kizalendo, ushindani utakuwa mkubwa zaidi baina ya bendi za Kizalendo, Wakongo hawana nafasi.

Wana kazi ngumu ya kusimama na kuhimili ushindani uliopo sasa, wenyewe wanajua nini kinaendelea,alisema Choki ambaye kundi lake lina wasanii kama Banza Stone, Super Nyamwela, Aisha Madinda na Ferguson.

 
                             

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Uplink Servers Technology | Bloggerized by Kwetu Bongo Online Magazine