Tuesday, October 1, 2013

Watu milioni 774 duniani ni mbumbumbu

Wakati kiwango cha watu wazima wasiojua kusoma na kuandika kikiongezeka kwa asilimia nane kuanzia mwaka 1990, taarifa ya utafiti mpya inasema bado kuna watu milioni 774 duniani wasiojua kusoma wala kuandika.

 

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Elimu, Sayansi na Utamaduni Unesco, lilitoa ripoti wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kujua Kusoma na Kuandika Septemba nane mwaka huu, iliyosema idadi kubwa ya watu hao mbumbumbu wanaishi katika mabara ya Afrika na Asia.
Pia takwimu za ripoti zinaonyesha kuwa robo tatu ya wale wasiojua kusoma na kuandika ni wanawake, na kwamba hali hiyo inaweza kuongezeka hata wakati wa kufikiwa tarehe ya mwisho ya malengo ya Maendeleo ya Milenia ambayo ni mwaka 2015.
Katika ujumbe wake kuadhimisha siku hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Unesco Irina Bokova  alisema kuwa dunia inapaswa kujikagua upya.
Alisema kuwa dunia ina wajibu wa  kuboresha mifumo yake ya utoaji wa elimu, kwani bila kufanya hivyo kuna uwezekano wa kurudi  nyuma kimaendeleo. “ Tunapaswa kumulika mifumo yetu ya utoaji elimu ili iende sambamba na mahitaji ya wakati” anasema.
Wasiojua kusoma na kuandika Tanzania
Ripoti hiyo ya Unesco imetolewa katika wakati ambapo kiwango cha kujua kusoma na kuandika nchini kikitajwa kuporomoka.Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2002 idadi ya Watanzania wasiojua kusoma na kundika ilifikia milioni 6.2.
Akizungumza bungeni, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa  idadi hiyo ni kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea, sawa na asilimia 31.
Aliongeza kusema kuwa  kuna uwezekanano idadi hiyo ikaongezeka kutokana na mazingira yaliyopo sasa.
Alieleza kuwa watu wasiojua kusoma na kuandika hawajamalizika, na kwamba Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012  bado haikuwa imetoa  mchanganuo wa watu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu.
“Ili kuimarisha Elimu ya Watu Wazima, Serikali inatekeleza mambo mbalimbali, ikiwemo kuboresha mpango wa awali wa Elimu ya Watu Wazima kupitia programu ya ‘Ndiyo Naweza’ yenye lengo la kupunguza idadi ya wasiojua kusoma na kuandika nchini’’ anasema na kuongeza:
“Serikali inatumia uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa Mpango wa Uwiano Kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (MUKEJA), ambapo mpaka mwaka 2012 ulikuwa na jumla ya wanakisomo 907,771.’’

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Uplink Servers Technology | Bloggerized by Kwetu Bongo Online Magazine