
KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Haruna Moshi ‘Boban’ (pichani)na beki, Godfrey Taita wametimuliwa kwenye kambi ya timu hiyo kutokana na utovu wa nidhamu.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya kambi hiyo, kimeliambia Championi Jumatatu kuwa Kocha Mkuu Charles Boniface Mkwasa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ wamefikia uamuzi wa kuwatimua Boban kutoka Simba na Taita wa Yanga.
“Boban aliondoka kwenye benchi wakati Stars inacheza na Zimbabwe, lakini Taifa amefanya kitu cha ajabu sana. Amekutwa na mwanamke chumbani kwake, ni hatari sana,” chanzo kililieleza Championi Jumatatu jana mchana.
“Unajua Taita alitaka kufanya ujanja lakini Julio ndiye alimkuta, tena si nje, huyo mwanamke alikuwa chumbani kwake. Haijajulikana ni changudoa au vipi!
“Boban aliinuka na kuondoka kwenye benchi kabla hata mechi kati ya Stars dhidi ya Zimbabwe kwisha, hali hiyo ilionyesha kuwaudhi mashabiki ambao walianza kumzomea.
Kuhusiana na sakata hilo, jana mchana, Mkwasa alisema: “Kweli tumemtimua Boban, tulikaa naye pamoja na kuhoji kuhusiana na tukio la yeye kuondoka kwenye benchi. Hakuwa na jibu la kuridhisha, maana alisema aliamua tu kuondoka. Tukaona ni utovu wa nidhamu, tumemfukuza.
“Kuhusu Taita, kweli nimesikia tukio hilo, sasa ndiyo niko njiani nakwenda kambini na kama tukithibitisha basi tutachukua hatua kali sana kwake.”
Kili Stars ambao ni mabingwa watetezi Stars wameweka kambi katika hoteli ya Rainbow jijini Dar es Salaam na wamekuwa wakienda mwendo wa kusua katika michuano ya Chalenji. Wamevuka hadi robo fainali kama ‘best looser’ baada ya kupoteza mechi mbili na kushinda moja tu.
0 comments:
Post a Comment