TIMU
ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes
leo imeanza vibaya kampeni za kuwania kucheza Fainali za Afrika kwa
vijana wenye umri huo, zitakazofanyika nchini Algeria mwakani, baada ya
kufungwa na Nigeria mabao 2-1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hadi
mapumziko, Nigeria, Flying Eagles walioonekana kutumia wachezaji
waliozidi umri, walikuwa mbele kwa mbele kwa mabao 2-0 katika mchezo huo
wa kwanza wa Raundi ya pili, yote yakitiwa kimiani na mshambuliaji wa
Enugu Rangers, Achaji Gero katika dakika ya pili na 44.
Kipindi
cha pili, Ngorongoro walibadilika na kucheza vizuri, wakiwazidi
wapinzani wao kumiliki mpira na kasi ya mchezo na hatimaye wakafanikiwa
kupata bao la kufutia machozi, lililofungwa na Atupele Green dakika ya
50, akimalizia krosi ya Ramadhani Singano ‘Messi’.
Ngorongoro
wangeweza kupata mabao zaidi, kama wangecheza soka ya chini, lakini
kutia krosi za juu kwenye lango la Nigeria ilikuwa ni kuwatesa
washambuliaji wao wafupi, Atupele na Simon Msuva.
Kwa
matokeo hayo sasa, Ngorongoro wanahitaji ushindi wa angalau wa mabao
2-0 katika mchezo wa marudiano Nigeria wiki mbili zijazo, ili kusonga
mbele.
Baada
ya mchezo huo, kocha wa Ngorongoro Heroes, Mdenmark Jakob Michelsen
alisema kwamba ataongeza nguvu katika kikosi chake kwa kuwaita wachezaji
wawili wanaocheza nje, kiungo Adam Nditi wa Chelsea na Thomas Ulimwengu
wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
sambamba na nyota wengine waliokwenda Ujerumani n TSU kwenye michuano ya
Fallerhof.
Katika
mchezo, kikosi cha Ngorongoro kilikuwa; Barwany Khomein, Omega Seme,
Jamal Mroki, Issa Rashid, Ruhana Samir, Yarouk Ramadhan, Kheri
Salum/Jerome Lambele, Frank Damayo, Simon Msuva, Atupele Green na
Ramadhan Singano.
Flying
Eagles; Samuel Okani, Hassan Abubakar, Ahiyu Mohamed, Ikechukwu Okine,
Chizoba Amaefule, Agboyi Oubokha, Moses Orkuma, Chidi Osochukwu, Yahaya
Adam/Harrison Egbune, Achaji Gero na Aminu Omar/Uchw Agbo.
Picha kwa hisani ya mdau Dina Ismail wa : http://dinaismail.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment